MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, anayeunda kundi la Wateule,
Taikuni Ally ‘Moxie’ jana amejitolea kuwasafirisha abiria bure kwenye
maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Moxie amejikuta akisukumwa kuwasafirisha abiria maeneo mbalimbali
ikiwa ni sehemu moja wapo ya
kurudisha kwa jamii, kutokana na kile
anachokifanya.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Moxie alieleza kuwa ameamua kukodi
UDA moja kwa ajili ya kuwasafirisha abiria bure sehemu yoyote Dar es
Salaam pale penye shida ya usafiri kwa siku nzima, lengo lake ikiwa ni
kurudisha kwa jamii kutokana na kile anachokiamini kuwa bila mashabiki
wake yeye asingekuwepo kwenye gemu la muziki.
Akizungumzia kwa nini ameamua kutoa huduma hiyo kwa siku ya Jumapili
na asifanye siku ya Jumatatu ambayo watu wengi wanaamini kuwa ndiyo siku
ambayo inashida ya usafiri hapa jijini, Moxie alisema kuwa kila siku
jijini kuna shida ya usafiri na yeye amepata nafasi ya kutoa huduma hiyo
kwa siku ya jana.
“Leo nazunguka jiji zima la Dar es Salaam, pale ambapo kunashida ya
usafiri ndipo tunapowapeleka abiria bure ikiwa ni sehemu moja wapo ya
kurudisha kwa jamii kutokana na kile wanachonifanyia hususani kwenye
muziki wangu” alisema Moxie.
“Mashabiki wangu ndio wanaosababisha mimi niendelee kuwepo kwenye
muziki na wao ndio wa kwanza kuingia katika shoo zangu, na hata kununua
albamu zangu hivyo kufanya hivi ni jambo ambalo ni sahihi ingawa
sitowafikia wote” aliongezea Moxie
Moxie ni msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini miondoko ya Hip Hop ,
aliyekuwa ndani ya kundi la Wateule, ambaye alikuwa akitamba na nyimbo
inayojulikana ‘watu kibao’.
