Safari za ndege za ndani ya nchi nchini Kenya
zinatarajiwa kurejea kama kawaida baadaye leo baada ya moto mkubwa
kuteketeza sehemu ya uwanja rasmi wa kimataifa wa ndege nchini humo
JKIA.
Msemaji wa ikulu ya rais, Manoah Esipisu alisema
kuwa ndege za mizigo zitaanza kusafiri lakini akaongeza kuwa serikali
haiwezi kusema bayana ni lini safari za kimataifa za ndege zitarejea
kama kawaida.
"Tunatarajia kuwa safari za ndege ndani ya nchi zitaweza kurejea kama kawaida baadaye leo, '' alisema Esipisu.
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta
awali leo ulikua umefungwa baada ya moto mkubwa kutokea katika uwanja
huo mjini Nairobi. Moto huo hata hivyo ulidhibitiwa
Hakuna ripoti zozote za majeruhi .
Mwandishi wa BBC katika uwanja huo amesema kuwa kulikuwa na moshi mkubwa uliotoka katika eneo la kuondokea na kuingilia wageni.
Baadhi ya safari za ndege kutoka uwanja huo pia ziliahirishwa wakati zengine zikielekezwa kwenda Mjini Mombasa.
Mwishoni mwa wiki jana baadhi ya wenye maduka ya
Duty Free katika uwanja huo walifurushwa baada ya serikali kusema kuwa
leseni za wenye maduka zilikuwa zimepitwa na muda.
Huu ni moto mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa
katika uwanja wa Jomo Kenyatta wenye kutumiwa na wasafiri wengi zaidi
katika eneo la Afrika mashariki na kati .
Taarifa za awali zilionyesha kuwa moto huo
ulianzia kwenye eneo la uhamiaji katika kitengo cha kupokea wageni kabla
ya kusambaa hadi maeneo ya ushuru na mizigo ya abiria.
Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana , lakini
maafisa wa ngazi ya juu wa serikali wakiongozwa na rais Uhuru Kenyatta
walitembelea uwanja huo na kutoa wito uchunguzi ufanyike mara moja. Hata
hivyo hawakutoa ishara yoyote ni lini uwanja huo utafunguliwa tena .
Shirika la ndege la kenya -Kenya Airways, ambalo
ni kubwa zaidi katika kanda ya Afrika limefuta safari zake zote na
kuelekeza ndege zinazoingia nchini katika mji wa Mombasa . Tayari hisa
za ndege zimeshuka kwa kiwango cha asilimia 2 . Ndege za kimataifa
ambazo zilitakiwa kuondoka leo asubuhi ziliruhusiwa kuondoka bila
wasafiri.

