![]() |
| Askari akikagua gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na Joan Kagezi |
Watu wenye silaha wamemuua mwendesha
mashitaka mkuu katika kesi ya watuhumiwa wa Kiislam wanaotuhumiwa kuua
watu kadha katika mashambulio ya bomu mwaka 2010.
Mwendesha
mashitaka huyo Joan Kagezi ambaye alikuwa kaimu mkurugenzi mwendesha
mashitaka msaidizi nchini Uganda ameuawa kwa kupigwa risasi na watu
waliokuwa katika pikipiki wakati akiendesha gari kurudi nyumbani mjini
Kampala.
Kesi inayoendelea inawahusu watu kumi na watatu wanaotuhumiwa kuwa wapiganaji wa kikundi cha al-Shabaab.
Wanatuhumiwa
kuua watu zaidi ya sabini wakati wakiangalia Fainali za Kombe la Dunia
za mwaka 2010 katika mgahawa mmoja na katika uwanja wa klabu ya rugby.
Wiki
iliyopita Marekani ilisema ilipata "habari za kuwepo uwezekano wa
shambulio" katika maeneo ya mji ambayo raia wa mataifa ya magharibi
wanakutana.
Serikali ya Uganda imesema Marekani ilionya juu ya uwezekano wa kuwepo kwa mtu anayejitoa mhanga akijaribu kuingia nchini humo.
Msemaji
wa serikali amesema Uganda ilikuwa katika kitisho kwa sababu imechangia
askari wengi katika jeshi la Umoja wa Afrika linalolinda amani nchini
Somalia wakipambana na kundi la al-Shabab ndani ya Somalia.


0 comments:
Post a Comment