![]() |
| Ummul-Khayr Sadir Abdul (19) |
Vyombo vya usalama nchini Kenya,
vinawashikilia wasichana watatu akiwamo Mtanzania, kwa kile kunachodaiwa
kutaka kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Somalia.
Taarifa
kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la El -Wak, mpakani mwa Kenya na
Somalia, Nelson Marwa amesema Mtanzania aliyekamatwa, alijieleza kuwa ni
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, Sudan.
Mtanzania
huyo, Ummul-Khayr Sadir Abdul (19), mwenyeji wa Zanzibar, anatajwa kuwa
kiongozi wa kundi hilo lililopanga kujiunga na al-Shabaab.
Wasichana wengine waliokamatwa pamoja na Ummul-Khayr, ni Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir wote raia wa Kenya.
“Hawa
wasichana watatu, inaaminika kuwa walikuwa wanakwenda Somalia kupata
mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga,”
alisema Kamishna Marwa.
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi
wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athumani alisema: “Tunafuatilia
hatujapokea taarifa zaidi ya hizo.”
Kamishna Marwa alisema raia
hao wawili wa Kenya, mmoja ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya
kilichopo Thika, Jimbo Kiambu na mwingine ni mwanafunzi wa Sekondari ya
Burhania, iliyopo Malindi, Kilifi.
“Serikali imepata taarifa
kuhusu watu wanaokusanya watu kutoka Afrika Mashariki ili wakajiunge na
makundi ya ugaidi nchini Somalia, wakala wetu wa usalama wamepata
taarifa hizo na kufanikisha kukamatwa kwa wasichana hao,” alisema
Kamishana Marwa.
Hivi karibuni, tovuti ya al-Jazeera ilitoa
taarifa za kukamatwa kwa mkanda wa video ulioonyesha mwakilishi wa kundi
la kigaidi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Levant (ISIL) akimtaka
kiongozi wa kundi la al-Shabaab kuliimarisha kwa kufanya mashambulizi ya
kigaidi katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Kamishna Marwa
alisema ingawa nyaraka za wasichana hao zote zinaonyesha kuwa ni
wanafunzi, lakini bado walibanwa kwa maswali kuhusu sababu inayowapeleka
nchini Somalia.
Aliongeza zaidi kuwa chanzo cha habari cha
kiusalama kilieleza kuwa nyaraka za wasichana hao zilionyesha kuwa
walikuwa wakienda kuolewa na wanajeshi wa kundi la al-Shabaab.


0 comments:
Post a Comment