Maafisa wa utawala Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati,
wamebana matumizi ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi baada ya kusema
kuwa ni tisho kwa usalama wa nchi.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa waziri wa mawasiliano serikali.
Watumiaji wa simu za mkononi ambao wamekuwa wakijaribu kutuma ujumbe mfupi wanapata jibu hili: ''Ujumbe wako hauwezi kutumwa.''
''Wenye simu za mkononi hawaruhusiwi kutuma
ujumbe mfupi kuanzia Jumatatu 2 Juni hadi itakapotolewa taarifa zaidi
kuhusu agizo hili,'' huu ndio ulikuwa ujumbe wa wizara ya mawasiliano
kwa kampuni za kutoa huduma za simu.
Inaarifiwa kuwa uamuzi huo ulifikiwa na waziri mkuu Andre Nzapayeke.
Tangu wiki iliyopita, kumekuwa na ghasia zaidi
mjini Bangui, pamoja na kutolewa wito wa maandamano uliotumwa kwa simu
kama ujumbe mfupi siku chache zilizopita.
Duru zinasema kuwa hatua ya kubana ujumbe mfupi wa simu itadumu kwa siku kadhaa kabla ya agizo lengine kubatilisha amri hiyo.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo inakumbwa na
vita kati ya jamii za wakristo na waisilamu imekuwa ikikumbwa na hali
ngumu ya usalama pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya jamii
hizo.

0 comments:
Post a Comment