![]() | |
|
Polisi nchini Kenya wanachunguza mauaji ya mwanajeshi
wa zamani wa Uingereza, ambaye aliuawa na genge la majambazi nyumbani
kwake mjini Nanyuki, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
David Parkinson na mkewe walishambuliwa na genge la majambazi waliokuwa wamejihami kwa silaha nyumbani kwaki siku ya Jumapili.
Bi Parkinson alinusurika baada ya kujificha katika chumba maalum ambacho genge hilo halikufanikiwa kubomoa.
Parkinson, ambaye alikuwa kamanda wa jeshi la
Uingereza lililoko mjini Nanyuki, ni mkulima mashuhuri na hujihusisha na
ufugaji wa ng'ombe.
Kwa mujibu wa afisa mkuu anayeongoza uchunguzi
huo, katika kaunti ya Laikipia, Marius Tum, genge la majambazi wapatao
watano waliingia nyumba ya afisa huyo wa zamani wa jeshi la Uingereza
baada ya kubomoa mlango mwendo wa saa saba za usiku wakati jamaa ya
marehemu walikuwa uzingizini.
Wakati wa makabiliano hayo, Parkinson alijeruhiwa vibaya na mkono wake mmoja ulikatwa kwa panga.
Genge hilo linasemekana lilimfunga Bi Parkinson
kwa kamba lakini alifanikiwa kutoroka na kujificha katika chumba hicho
maalum, wakati huo mumewe alikuwa akivuja damu sakafuni.
Na wakati alipojitokeza baada ya wezi hao kutoroka alikuta mumeo tayari alikuwa ameaga dunia.
Idara ya polisi imesema kuwa wezi hao waliiba
kiasi kisichojulikana cha pesa pamoja na simu moja ya mkononi,
tarakilishi na vifaa vingine vya nyumbani.
Maafisa wanachunguza mauaji hayo tayari wamemkamata mshukiwa mmoja.
Parkinson alitumikia jeshi la Uingereza na
kupanda hadi cheo cha Luteni Kanali na alituzwa na Malkia wa Uingereza
mwaka wa 1998 kwa juhudi zake katika jeshi la nchi hiyo.

