![]() |
| Raia wakibeba mwili wa mtu aliyeuawa Goma |
Mapigano mapya yamezuka mwishoni mwa juma katika eneo
la Goma, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo ripoti
zinasema watu watatu walifariki baada ya makombora kurushwa katika
maeneo ya makaazi ya watu.
Haijulikani ni nani aliyerusha makombora hayo
lakini wanainchi wameandamana wakililaumu jeshi la kulinda amani la
Umoja wa Mataifa MONUSCO kwa kile wanachodai limewashambulia waasi
katika juhudi za kuwatimua kwenye eneo hilo.
Wanajeshi
wa Umoja wa Mataifa wamewalaumu waasi kwa kurusha makombora hayo lakini
hakuna kundi lolote la waasi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo.
Afrika Kusini, ambayo imechangia kikosi hicho
cha kulinda amani, imekiri kuwa mwanajeshi wake mmoja amejeruhiwa katika
mlipuko huo wa bomu.
Akizungumza kwa simu na BBC, Msemaji wa jeshi la
Afrika Kusini, Brigedia Generali Kolani Mabanga, amesema mwanajeshi
wake mmoja alijeruhiwa vibaya na kwa sasa anaendelea kupata matibabu
huku mipango ya kumrejesha nyumbani kwa matibabu zaidi ikiendelea.
Hali ya ulinzi imeimarisha katika eneo hilo lakini wakaazi wa mji huo na viunga vyake wanasema hali bado ni ya wasi wasi.

