Rais wa mpito nchini Misri, anasema kuwa juhudi za
kimataifa kutuliza mgogoro wa kisiasa nchini humo ambao ulitokana na
kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Rais Mohammed Morsi, zimegongwa
mwamba.
Adly Mansour na washirika wake walioko kwenye
jeshi, wamekuwa wakishauriana na wajumbe wa kimataifa kutoka Marekani,
Muungano wa Ulaya , Qatar na Milki za kiarabu.
Zaidi ya watu 250 wameuawa kwenye
mgogoro huo wa kisiasa tangu Morsi kuondolewa mamlakani tarehe 3 mwezi
Julai baada ya maandamano ya umma.
Maseneta wawili wa Marekani siku ya Jumanne waliitisha mazungumzo kati ya serikali ya mpito na vuguvugu la Muslim Brtherhood
Lakini serikali ya mpito hii leo ilitangaza kuwa mazungumzo ya kidiplomasia yamefika kikomo leo.
Iliongeza kusema kuwa juhudi hizo hazijafanikisha chochote.
Brotherhood walaumiwa
Serikali imesema kuwa inalaumu vuguvugu la
Muslim Brotherhood kwa kutofanikiwa kwa juhudi za amani na matukio
mengine yanayohusu utovu wa usalama na ukiukwaji wa sheria.
Mjumbe wa Marekani Bernardino Leon na mwenzake
naibu waziri wa mambo ya nje wamekuwa Misri kwa siku kadhaa kufanya
mazungumzo ya kupatanisha pande hizi mbili katika mgogoro huu.
"tutajaribu kadri ya uwezo wetu kuhakikisha watu wanashauriana,'' alisema msemaji wa EU Michael Mann.
"ni Muhimu kuona kuwa kunakuwa na kipindi cha
mpito chenye kuzingatia demokrasia...tutaendelea na juhudi zetu,''
aliongeza msemaji huyo.
Waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi amekuwa
mjumbe wa hivi karibuni aliyetarajiwa kufanya mzungumzo na mwenzake wa
Misri, waziri mkuu na rais wa mpito pamoja na maafisa wengine mnamo
Jumatano

